Tehrik-e Taliban Pakistan (TTP) ni kundi la kigaidi lenye makao yake nchini Pakistani na Afuganistani lililoanzishwa mnamo mwaka 2007. TTP inanuia kuisukuma serikali ya Pakistani kutoka Mkoa wa Khyber Pakhtunkwa (zamani ukijulikana kama Maeneo ya Kikabila Yaliyosimamiwa na Shirikisho) na kuanzisha utawala wa sharia kupitia vitendo vya kigaidi. TTP hupata mwongozo wa kiitikadi kutoka kwa al-Qa’ida (AQ), huku wanachama wa AQ wakiitegemea TTP kwa kiasi fulani maficho salama kwenye maeneo yaliyo karibu na mpaka kwa Afuganistani na Pakistani. Mpango huu umeipa TTP uwezo wa kuufikia mtandao wa kimataifa wa kigaidi wa AQ na ujuzi wa kiutendaji wa wanachama wake.
TTP imetekeleza na kudai kuhusika na vitendo vingi vya kigaidi dhidi ya maslahi ya Pakistani na Marekani, likiwamo shambulio la bomu la kujitoa mhanga la mwezi Disemba, mwaka 2009 kwenye kambi ya kijeshi ya Marekani, eneo la Khost, nchini Afuganistani ambalo liliwaua raia saba wa Marekani, na vilevile shambulio la bomu kujitoa mhanga mnamo mwezi Aprili, mwaka 2010 dhidi ya Ubalozi Mdogo wa Marekani eneo la Peshawar, Pakistani, ambalo liliwaua raia sita wa Pakistani. TTP inashukiwa kuhusika na mauaji ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Pakistan, Benazir Bhutto, mnamo mwaka 2007. TTP ilielekeza na kufadhili jaribio lililoshindikana la Faisal Shahzad kulipua kifaa kilipuzi katika eneo la Times Square jijini New York mnamo tarehe mosi, mwezi Mei, mwaka mwaka 2010.
Mnamo tarehe mosi, mwezi Septemba, mwaka 2010, Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Marekani ilitaja TTP kuwa Kundi la Kigaidi la Kigeni chini ya kifungu 219 cha Sheria ya Uhamiaji na Uraia, kama ilivyorekebishwa, na kama Gaidi wa Kimataifa Mwenye Sifa Maalumu kuambatana na Amri ya Rais 13224, kama ilivyorekebishwa. Matokeo yake ni kwamba, mali yote na maslahi ya TTP katika mali, vyote vilivyoko chini ya mamlaka ya Marekani vimezuiwa, na watu wa Marekani kwa jumla wamekatazwa kushiriki kwenye miamala yoyote na TTP. Ni kosa la jinai kutoa kwa makusudi, au kujaribu au kula njama ya kutoa, msaada wa nyenzo au rasilimali kwa TTP.