Taifa la Kiislamu Nchini Iraki na Syria (ISIS) iliibuka kutoka kwa masalio ya al-Qa’ida Nchini Iraki (AQI). Kundi hilo lilijipa jina la ISIS ili kuelezea matamanio yake ya kieneo ikipanua shughuli kujumuisha mzozo wa Syria. ISIS iliongozwa na Abu Bakr al-Baghdadi, aliyetangaza kuanzishwa kwa khalifa ya Kiislamu mnamo mwezi Juni, mwaka 2014. Aliuliwa mnamo tarehe 27 mwezi Oktoba, mwaka 2019 wakati wa operesheni ya kijeshi ya Marekani ya kumkamata. ISIS ilitumia mzozo wa Syria na uhasama wa makundi mbalimbali nchini Iraki, ambao uliiruhusu kupata udhibiti wa eneo la ardhi kwenye nchi zote mbili. Mnamo mwaka 2019, Muungano wa Kimataifa Kuishinda ISIS – ukijumuisha mataifa kadha washirika na taasisi za kimataifa – ulikomboa eneo lote lililodhibitiwa na ISIS nchini Syria na Iraki. Harakati dhidi ya kundi hilo Iraki, Syria, na nchi zingine zinaendelea.
Mnamo mwezi Novemba, mwaka 2015, ISIS ilitekeleza jijini paris mashambulio kadha yaliyoratibiwa ambayo yaliwaua watu karibu 130, akiwamo Mmarekani, na kujeruhi wengine zaidi ya 350. Mnamo mwezi Machi, mwaka 2016, ISIS ilielekeza mashambulio mawili kwa wakati mmoja jijini Brussels ambayo yaliwaua watu 32, wakiwamo raia wanne wa Marekani, na kujeruhi watu zaidi ya 250. Mnamo mwezi Juni 2016, mshambuliaji mwenye bunduki aliyeahidi utii kwa ISIS aliwaua watu 49 na kuwajeruhi wengine 53 kwenye klabu ya usiku ya Pulse mjini Orlando, Florida. Mnamo mwezi Julai, mwaka 2016, ISIS ilidai kuhusika na shambulio ambapo gaidi akiendesha lori la mizigo alishambulia umati wa watu mjini Nice, Ufaransa, wakati wa sherehe za Siku ya Bastille, na kusababisha vifo vya watu 86, wakiwamo raia watatu wa Marekani. Mnamo mwezi Januari mwaka 2019, ISIS ilidai kuhusika na shambulio la bomu la kujitoa mhanga dhidi ya mkahawa mmoja mjini Manbij, Syria, ambalo liliwaua watu 19, wakiwamo Wamarekani wanne. Mnamo Jumapili ya Pasaka mwaka 2019 nchini Sri Lanka, watu zaidi ya 250 waliuliwa, wakiwamo raia watano wa Marekani, wakati magaidi waliotiwa moyo na ISIS walitekeleza mashambulio ya mabomu ya kujitoa mhanga yaliyoratibiwa kwenye makanisa na hoteli kadha.
Mnamo tarehe 17 mwezi Disemba, mwaka 2004, Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Marekani ilitaja AQI (inayojulikana sasa kama ISIS) kuwa Kundi la Kigaidi la Kigeni chini ya kifungu 219 cha Sheria ya Uhamiaji na Uraia, kama ilivyorekebishwa. Hapo awali, mnamo tarehe 15 mwezi Oktoba, mwaka 2004, Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje iliitaja AQI kuwa Gaidi wa Kimataifa Mwenye Sifa Maalumu kuambatana na Amri ya Rais 13224, kama ilivyorekebishwa. Matokeo yake ni kwamba, mali yote na maslahi ya ISIS katika mali, vyote vilivyoko chini ya mamlaka ya Marekani vimezuiwa, na watu wa Marekani kwa jumla wamekatazwa kushiriki kwenye miamala yoyote na ISIS. Ni kosa la jinai kutoa kwa makusudi, au kujaribu au kula njama ya kutoa, msaada wa nyenzo au rasilimali kwa ISIS.