Tuzo kwa Mahakama inaahidi kutoa tuzo ya hadi dola milioni kumi kwa taarifa kumhusu Sirajuddin Haqqani, anayejulikana pia kama Siraj Haqqani na Khalifa. Sirajuddin huongoza Mtandao wa Haqqani (HQN), kundi lililotajwa na Marekani kama Shirika la Kigaidi la Kigeni (FTO). Chini ya uongozi wake, HQN imepanga na kutekeleza mara nyingi utekaji nyara na mashambulio makuu dhidi ya vikosi vya Marekani na Muungano nchini Afuganistani, serikali ya Afuganistani, na shabaha za kiraia. Mnamo mwaka 2015, Sirajuddin aliteuliwa naibu kiongozi wa Talibani, hatua iliyoimarisha muungano kati ya HQN na Talibani.
Wakati wa mahojiano na shirika moja la habari la Marekani, Sirajuddin alikiri kupanga shambulio la tarehe 14 mwezi Januari, mwaka 2008 dhidi ya Hoteli ya Serena mjini Kabul, nchini Afuganistani, ambalo liliwaua watu sita, akiwamo raia wa Marekani Thor David Hesla. Sirajuddin pia alikiri kwamba alipanga jaribio la mwezi Aprili, mwaka 2008 la kumuua Rais wa Afuganistani Hamid Karzai.
Mnamo tarehe 11 mwezi Machi, mwaka 2008, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilimtaja Sirajuddin Haqqani kama Gaidi wa Kimataifa Mwenye Sifa Maalumu kuambatana na Amri ya Rais 13224, kama ilivyorekebishwa. Matokeo ya kutajwa huku, miongoni mwa matokeo mengine, ni kwamba mali yote na maslahi ya Sirajuddin katika mali, vyote vilivyoko chini ya mamlaka ya Marekani vimezuiwa, na watu wa Marekani kwa jumla wamekatazwa kushiriki kwenye miamala yoyote na Sirajuddin. Aidha, ni kosa la jinai kutoa kwa makusudi, au kujaribu au kula njama ya kutoa, msaada wa nyenzo au rasilimali kwa FTO HQN.