Tuzo kwa Mahakama inaahidi kutoa tuzo ya hadi dola milioni kumi kwa taarifa kumhusu Muhammad al-Jawlani, ambaye pia anajulikana kama Abu Muhammad al-Golani na Muhammad al-Julani. Al-Jawlani huongoza Vuguvugu la al-Nusrah (ANF), mshirika wa al-Qa’ida’s (AQ) nchini Siria. Mnamo mwezi Januari 2017, ANF liliungana na makundi mengine kadha ya upinzani yenye msimamo mkali kuunda Hayat Tahrir al-Sham (HTS). Ijapokuwa al-Jawlani siye kiongozi wa HTS, angali ni kiongozi wa ANF, mshirika wa AQ na msingi wa HTS.
Chini ya uongozi wa al-Jawlani, ANF imetekeleza mashambulio mengi ya kigaidi kote nchini Siria, mara nyingi ikiwalenga raia. Mnamo mwezi Aprili, mwaka 2015, inasemekana ANF iliwateka nyara, na baadaye kuachilia huru, yapata raia 300 wa Kikurdi kwenye kituo cha ukaguzi wa magari barabarani nchini Siria. Mnamo mwezi Juni, mwaka 2015, ANF lilidai kuhusika na mauaji ya wakazi 20 wa kijiji cha Druze, eneo la Qalb Lawzeh mkoani Idlibu, Siria.
Mnamo mwezi Aprili, mwaka 2013, al-Jawlani aliahidi utii kwa AQ na kiongozi wake Ayman al-Zawahiri. Mnamo mwezi Julai, mwaka 2016, al-Jawlani alisifu AQ na al-Zawahiri katika video ya mtandaoni na akadai ANF ingebadilisha jina lake kuwa Jabhat Fath Al Sham (“Kikosi cha Ushindi Levant”).
Mnamo tarehe 16 mwezi Mei, mwaka 2013, Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Marekani ilimtaja al-Jawlani kama Gaidi wa Kimataifa Mwenye Sifa Maalumu kuambatana na Amri ya Rais 13224, kama ilivyorekebishwa. Matokeo ya kutajwa huku, miongoni mwa matokeo mengine, ni kwamba mali yote na maslahi ya al-Jawlani katika mali, vyote vilivyoko chini ya mamlaka ya Marekani vimezuiwa, na watu wa Marekani kwa jumla wamekatazwa kushiriki kwenye miamala yoyote na al-Jawlani. Aidha, ni kosa la jinai kutoa kwa makusudi, au kujaribu au kula njama ya kutoa, msaada wa nyenzo au rasilimali kwa ANF, kundi lililotajwa na Marekani kama Shirika la Kigaidi la Kigeni.