Tuzo kwa Mahakama inaahidi kutoa tuzo ya hadi dola milioni tano kwa taarifa kuhusu mitandao ya utekaji nyara ya ISIS au kwa taarifa zitakazowezesha kutambuliwa waliko, kuokolewa, na kurejeshwa kwa Maher Mahfouz, Michael Kayyal, Gregorios Ibrahim, Bolous Yazigi, na Paolo Dall’Oglio.
Mnamo tarehe 9 mwezi Februari, mwaka 2013, kasisi wa kanisa la Othodoksi la Ugiriki Maher Mahfouz na kasisi wa kanisa Katoliki la Armenia Michael Kayyal walikuwa ndani ya basi la umma wakisafiri kuelekea makao ya watawa na makasisi eneo la Kafrun, nchini Siria. Takribani kilometa 30 nje ya Aleppo, Siria, watu wanaoshukiwa kuwa wanachama wa ISIS wenye itikadi kali walisimamisha gari hilo, wakakagua hati za abiria, halafu wakawatoa Mahfouz na Kayyal kutoka kwenye basi hilo. Hawajaonekana wala kusikika tangu wakati huo.
Mnamo tarehe 22 mwezi Aprili, mwaka 2013, Askofu Mkuu wa kanisa la Othodoksi la Siria Gregorios Ibrahim alisafiri kutoka Aleppo hadi Uturuki kumchukua Askofu Mkuu wa kanisa la Othodoksi la Ugiriki Bolous Yazigi. Walipofika kwenye kituo cha ukaguzi wa magari barabarani karibu na al-Mansoura, nchini Siria, wanaume kadha waliokuwa na bunduki waliwavizia maaskofu hao na kutwaa gari lao. Dereva wa wahubiri hao alipatikana baadaye akiwa mfu. Maaskofu hao wanaaminika kuwa walitekwa nyara na watu walio na ushirika na al-Nusra Front, kundi mshirika wa al-Qa’ida;hata hivyo, maaskofu hao baadaye walihamishiwa kwa ISIS.
Mnamo tarehe 29 mwezi Julai, mwaka 2013, ISIS ilimteka nyara kasisi wa dhehebu la Jesuit la Italia Paolo Dall’Oglio kwenye eneo la Raqqah, nchini Siria. Padre Dall’Oglio alikuwa amepanga kukutana na ISIS ili kuomba kuachiliwa huru kwa Mahfouz, Kayyal, Ibrahim, na Yazigi. Hajaonekana wala kusikika tangu wakati huo.