Tuzo kwa Mahakama inaahidi kutoa tuzo ya hadi dola milioni tano kwa taarifa kumhusu Khalil al-Rahman Haqqani, anayejulikana pia kama Khalil Haqqani au Khalil Ahmad Haqqani. Khalil ni kiongozi muhimu wa Mtandao wa Haqqani (HQN), kundi lililotajwa na Marekani kama Shirika la Kigaidi la Kigeni (FTO).
Khalil hujihusisha na shughuli za kuchangisha pesa kwa niaba ya Talibani na hutoa usaidizi kwa Watalibani wanaoendesha shughuli zao nchini Afuganistani. Kufikia mapema mwaka 2010, alitoa pesa kwa vikundi vya Talibani Mkoa wa Logar, nchini Afuganistani. Mnamo mwaka 2009, Khalil alikuwa mmoja wa watu kadha waliokuwa na jukumu la kuwazuilia watu waliotekwa na Talibani na HQN. Khalil ametekeleza mashambulio kwa niaba ya Talibani kwa maagizo kutoka kwa mpwa wake, Sirajuddin Haqqani, aliye kiongozi mkuu wa HQN na naibu kiongozi wa Talibani. Khalil pia amefanya kazi kwa niaba ya al-Qa’ida (AQ) na amehusishwa na shughuli za kigaidi za AQ. Mnamo mwaka 2002, alipeleka wapiganaji ili kuwaimarisha nguvu wapiganaji wa AQ kwenye Mkoa wa Paktia, nchini Afuganistani.
Mnamo tarehe 9 mwezi Februari, mwaka 2011, Wizara ya Fedha ya Marekani ilimtaja Khalil Haqqani kama Gaidi wa Kimataifa Mwenye Sifa Maalumu kuambatana na Amri ya Rais 13224, kama ilivyorekebishwa. Matokeo ya kutajwa huku, miongoni mwa matokeo mengine, ni kwamba mali yote na maslahi ya Khalil Haqqani katika mali, vyote vilivyoko chini ya mamlaka ya Marekani vimezuiwa, na watu wa Marekani kwa jumla wamekatazwa kushiriki kwenye miamala yoyote na Khalil Haqqani. Aidha, ni kosa la jinai kutoa kwa makusudi, au kujaribu au kula njama ya kutoa, msaada wa nyenzo au rasilimali kwa FTO HQN.