Tuzo kwa Mahakama inaahidi kutoa tuzo ya hadi dola milioni 10 kwa taarifa kumhusu Jehad Serwan Mostafa, anayejulikana pia kama Ahmed Gurey, Anwar al-Amriki, na Emir Anwa. Mostafa ni raia wa Marekani na mkazi wa zamani wa California, ambaye ameshikilia nafasi za uongozi katika al-Shabaab, kundi lililotajwa na Marekani kama Shirika la Kigaidi la Kigeni. Anaaminika kuwa raia wa Marekani aliye na wadhifa mkubwa zaidi ambaye anapigana nje ya nchi katika shirika la kigaidi.
Mostafa aliishi na kufuzu kutoka chuo mjini San Diego, California, kabla ya kuhamia Somalia mnamo mwaka 2005. Inaaminika alishiriki katika mashambulio dhidi ya majeshi ya Ethiopia kabla ya kujiunga na al-Shabaab yapata mwaka 2008. Akiwa na al-Shabaab, Mostafa ametumika katika nafasi mbalimbali muhimu, ikiwamo kuhudumu kama mkufunzi wa kijeshi kwenye kambi za mafunzo za kundi hilo, kuwaongoza wapiganaji wa kigeni, kufanya kazi katika kitengo cha habari cha kundi hilo, kutumika kama mjumbe kati ya al-Shabaab na mashirika mengine ya kigaidi, na kuongoza matumizi ya vilipukaji ya kundi hilo katika mashambulio ya kigaidi. Mostafa anaaminika kuendelea kutekeleza jukumu muhimu katika kupanga mashambulio yanayoelekezwa dhidi ya serikali ya Somalia na majeshi yanayoungwa mkono kimataifa ya Muungano wa Afrika nchini Somalia na Afrika Mashariki. Kutokana na hilo, Mostafa anaendelea kuwa tishio la moja kwa moja kwa vikosi, raia, na maslahi ya Marekani.
Mnamo tarehe 9 mwezi Oktoba, mwaka 2009, Mostafa alifunguliwa rasmi mashtaka kwenye eneo la Wilaya ya Kusini ya mji wa California kwa mashtaka ya kula njama ya kuwapa magaidi msaada wa nyenzo, kula njama ya kutoa msaada wa nyenzo kwa al-Shabaab, na kutoa msaada wa nyenzo kwa al-Shabaab. Mnamo tarehe 2 mwezi Disemba, mwaka 2019, shtaka lenye makosa zaidi lililofunguliwa rasmi katika mahakama ya serikali kuu ya Marekani lilimshtaki Mostafa kwa makosa yaliyohusiana na ugaidi. Mostafa yupo kwenye Orodha ya Magaidi Wanaosakwa Zaidi ya Shirika la FBI.