Jamaat-ul-Ahrar (JuA) ni kundi la wapiganaji linaloshirikiana na lile la Tehrik-e Taliban Pakistan (TTP) lililotajwa na Marekani kama Kundi la Kigeni la Kigaidi. Kundi la JuA lililoanzishwa na kiongozi wa zamani wa TTP Abdul Wali mnamo mwezi Agosti, mwaka 2014, limefanya mashambulio mengi nchini Pakistani likilenga raia, waumini wa dini ndogo, wanajeshi, na maafisa wa kutekeleza sheria. Mnamo mwezi Agosti, mwaka 2015, JuA ilidai kuhusika na shambulio la kujitoa mhanga katika eneo la Punjab, Pakistani ambalo lilimuua Waziri wa Mambo ya Ndani wa Punjab Shuja Khanzada na wafuasi wake 18. JuA ilihusika na mauaji ya raia wawili wa Pakistani waliokuwa wafanyakazi wa Ubalozi Mdogo wa Marekani eneo la Peshawar mapema mwezi Machi, mwaka 2016. Mwishoni mwa mwezi Machi, mwaka 2016, JuA ilifanya shambulio la kujitoa mhanga kwenye bustani ya starehe ya Gulshan-e-Iqbal eneo la Lahore, Pakistani, ambalo liliwaua watu zaidi ya 70 — karibu nusu yao wakiwa wanawake na watoto —na kujeruhi mamia ya wengine.
Mnamo tarehe 3, mwezi Agosti, mwaka 2016, Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Marekani ilitaja JuA kuwa Gaidi wa Kimataifa Mwenye Sifa Maalumu kuambatana na Amri ya Rais 13224, kama ilivyorekebishwa. Matokeo yake ni kwamba, mali yote na maslahi ya JuA katika mali, vyote vilivyoko chini ya mamlaka ya Marekani vimezuiwa, na watu wa Marekani kwa jumla wamekatazwa kushiriki kwenye miamala yoyote na JuA.