Jama’at Nusrat al-Islam wal-Muslimin (JNIM) limejieleza kama tawi rasmi la al-Qa’ida nchini Mali. Mnamo mwaka 2017, tawi la Sahara la al-Qa’ida kwenye eneo la Kiislamu la Maghreb, al-Murabitoun, Ansar al-Dine, na Macina Liberation Front wote waliungana kuunda JNIM. Likiendesha shughuli zake nchini Mali, Nijeri, na Bukinafaso, JNIM limehusika na mashambulio mengi na utekaji nyara. Mnamo mwezi Juni, mwaka 2017, JNIM ilishambulia eneo maalum la mapumziko ya kitalii nje ya jiji la Bamako lenye kutembelewa sana na watu kutoka mataifa ya Magharibi na ilihusika na mashambulio makubwa yaliyoratibiwa jijini Ouagadougou mnamo tarehe 2 mwezi Machi, mwaka 2018. Mnamo mwezi Septemba, JNIM ililipua bomu la ardhini chini ya basi la abiria katikati mwa nchi ya Mali, likawaua raia 14 na kuwajeruhi wengine 24.
Mnamo tarehe 6 mwezi Septemba, mwaka 2018, Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Marekani ilitaja JNIM kuwa Kundi la Kigaidi la Kigenii chini ya kifungu 219 cha Sheria ya Uhamiaji na Uraia, kama ilivyorekebishwa. Hapo awali, mnamo tarehe 5 mwezi Septemba, mwaka 2018, Wizara ya Mambo ya Nje iliitaja JNIM kuwa Gaidi wa Kimataifa Mwenye Sifa Maalumu kuambatana na Amri ya Rais 13224, kama ilivyorekebishwa. Matokeo yake ni kwamba, mali yote na maslahi ya JNIM katika mali, vyote vilivyoko chini ya mamlaka ya Marekani vimezuiwa, na watu wa Marekani kwa jumla wamekatazwa kushiriki kwenye miamala yoyote na JNIM. Ni kosa la jinai kutoa kwa makusudi, au kujaribu au kula njama ya kutoa, msaada wa nyenzo au rasilimali kwa JNIM.