Hizballah ni kundi la kigaidi lenye makao yake nchini Lebanoni, ambalo hupokea silaha, mafunzo, na ufadhili kutoka Irani, ambayo Waziri wa mambo ya Nchi za Nje alitaja kuwa Taifa Linalofadhili Ugaidi mnamo mwaka 1984. Hizballah linadumisha mtandao mkubwa wa kigaidi na limehusika na mashambulio mengi makubwa. Hayo ni pamoja na: shambulio la mwaka 1983 la mabomu ya kujitoa mhanga yaliyotegwa kwenye lori dhidi ya Ubalozi wa Marekani Beirut na Kambi ya Jeshi la Wanamaji wa Marekani jijini Beirut;shambulio la mwaka 1984 dhidi ya jengo dogo lililounganishwa na Ubalozi wa Marekani Beirut;na utekaji nyara wa Ndege Nambari TWA 847 mnamo mwaka 1984. Hizballah pia ilihusishwa, pamoja na Irani, na mashambulio ya mwaka 1992 dhidi ya Ubalozi wa Israeli nchini Ajentina pamoja na lile la bomu la mnamo mwaka 1994 dhidi ya Ushirika wa Kutoa Misaada wa Kiyaudi Ajentina kwa jina Argentine Jewish Mutual Aid Society mjini Buenos Aires. Mnamo mwaka 2012, majasusi wa Hizballah walifanikiwa kutekeleza shambulio la bomu la kujitoa mhanga nchini Bulgaria. Maafisa wa kutekeleza sheria wamezuia majaribio ya mashambulio ya kigaidi na njama za Hizballah nchini kama vile Azabajani, Saiprasi, Misri, Kuwaiti, Nijeria, Peru, na Tailandi.
Mnamo tarehe 8 mwezi Oktoba, mwaka 1997, Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Marekani ilitaja Hizballah kuwa Kundi la Kigaidi la Kigeni chini ya kifungu 219 cha Sheria ya Uhamiaji na Uraia, kama ilivyorekebishwa. Baadaye, mnamo tarehe 31 mwezi Oktoba, mwaka 2001, Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Marekani iliitaja Hizballah kuwa Gaidi wa Kimataifa Mwenye Sifa Maalumu kuambatana na Amri ya Rais 13224, kama ilivyorekebishwa. Matokeo yake ni kwamba, mali yote na maslahi ya Hizballah katika mali, vyote vilivyoko chini ya mamlaka ya Marekani vimezuiwa, na watu wa Marekani kwa jumla wamekatazwa kushiriki kwenye miamala yoyote na Hizballah. Ni kosa la jinai kutoa kwa makusudi, au kujaribu au kula njama ya kutoa, msaada wa nyenzo au rasilimali kwa Hizballah.