Tuzo kwa Mahakama inaahidi kutoa tuzo ya hadi dola milioni kumi kwa taarifa kumhusu Hafiz Saeed, mwanzilishi na kiongozi wa Lashkar-e-Tayyiba (LeT), kundi lililotajwa na Marekani kama Shirika la Kigaidi la Kigeni (FTO). Saeed alishiriki katika kupanga shambulio la kigaidi kwa siku nne dhidi ya mji wa Mumbai, India mnamo mwezi Novemba, mwaka 2008 ambapo watu 166 waliuliwa, wakiwamo Wamarekani sita.
Mnamo mwaka 2020, mahakama ya kupambana na ugaidi ya Pakistani ilimpata Saeed na hatia kwa makosa mbalimbali ya kufadhili ugaidi na ikamhukumu kufungwa gerezani. Marekani inaendelea kutafuta taarifa kumhusu Saeed kwa sababu mfumo wa mahakama wa Pakistan umewaachilia huru viongozi na majasusi wa LeT waliopatwa na hatia hapo awali.
Mnamo tarehe 27 mwezi Mei, mwaka 2008, Wizara ya Fedha ya Marekani ilimtaja Saeed kama Gaidi wa Kimataifa Mwenye Sifa Maalumu kuambatana na Amri ya Rais 13224, kama ilivyorekebishwa. Matokeo ya kutajwa huku, miongoni mwa matokeo mengine, ni kwamba mali yote na maslahi ya Saeed katika mali, vyote vilivyoko chini ya mamlaka ya Marekani vimezuiwa, na watu wa Marekani kwa jumla wamekatazwa kushiriki kwenye miamala yoyote na Saeed. Aidha, ni kosa la jinai kutoa kwa makusudi, au kujaribu au kula njama ya kutoa, msaada wa nyenzo au rasilimali kwa FTO LeT. Mnamo tarehe 10 mwezi Disemba, mwaka 2008, Saeed aliorodheshwa kwenye Kamati ya Umoja wa Mataifa 1267/1989 ya Vikwazo vya al-Qa’ida kama mtu anayehusishwa na shirika la kigaidi la al-Qa’ida na, hivyo basi, yuko chini ya vikwazo vya kimataifa.