Al-Shabaab ni mshirika wa al-Qa’ida (AQ) na ina mahusiano na washirika wengine wa AQ, ikiwemo AQ kwenye Rasi ya Kiarabu na AQ eneo la Kiislamu la Maghreb. Al-Shabaab ilikuwa ndio mrengo wa wapiganaji wa lililokuwa Baraza la Mahakama za Kiislamu ambalo lilitwaa sehemu za kusini mwa Somalia nusu ya pili ya mwaka 2006. Tangu mwishoni mwa mwaka 2006, al-Shabaab na wanamgambo wanaoshirikiana nayo wameshiriki uasi wa matumizi ya nguvu kwa kutumia vita vya msituni na mbinu za kigaidi dhidi ya serikali ya mpito ya Somalia.
Al-Shabaab imefanya mashambulio nchini Somalia, Kenya, Uganda, na Jibuti. Al-Shabaab ilihusika na mashambulio ya mabomu ya kujitoa mhanga yaliyotokea jijini Kampala mnamo tarehe 11, mwezi Julai, mwaka 2010. Shambulio hilo, ambalo lilitokea wakati wa Kombe la Dunia, liliwaua watu 76, akiwamo raia wa marekani. Mnamo mwezi Septemba, mwaka 2013, al-Shabaab ilitekeleza shambulio kubwa dhidi ya jengo la maduka la Westgate Mall jijini Nairobi. Kuzingirwa kwa jengo hilo kulikoendelea kwa siku kadha kulisababisha vifo vya angalau raia 65, na vilevile wanajeshi na polisi sita na mamia ya wengine walijeruhiwa. Mnamo mwezi Aprili mwaka 2015, al-Shabaab ilifanya uvamizi Chuo Kikuu cha Garissa kwa kutumia bunduki ndogo na makombora ya gruneti ambao uliua watu 148.
Mnamo tarehe 18 mwezi Machi, mwaka 2008, Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Marekani ilitaja al-Shabaab kuwa Kundi la Kigaidi la Kigeni chini ya kifungu 219 cha Sheria ya Uhamiaji na Uraia, kama ilivyorekebishwa. Baadaye, Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Marekani ilitaja al-Shabaab kuwa Gaidi wa Kimataifa Mwenye Sifa Maalumu kuambatana na Amri ya Rais 13224, kama ilivyorekebishwa. Matokeo yake ni kwamba, mali yote na maslahi ya al-Shabaab katika mali, vyote vilivyoko chini ya mamlaka ya Marekani vimezuiwa, na watu wa Marekani kwa jumla wamekatazwa kushiriki kwenye miamala yoyote na al-Shabaab. Ni kosa la jinai kutoa kwa makusudi, au kujaribu au kula njama ya kutoa, msaada wa nyenzo au rasilimali kwa al-Shabaab.