Mwanzoni likijulikana kama Kundi la Kisalafi la Mahubiri na Vita, al-Qa’ida (GSPC) katika eneo la Kiislamu la Maghreb (AQIM) ilitokea baada ya kundi hilo kuahidi utii kwa al-Qa’ida mnamo mwaka 2006. Ingawa kwa kiasi kikubwa AQIM lingali kundi la kigaidi linaloendesha shughuli zake kwenye eneo la Sahel, limechukua matamshi na itikadi kali zaidi dhidi ya mataifa ya Magharibi.
Mara kwa mara AQIM imefanya vitendo vya ugaidi, ikiwemo mabomu ya kujitoa mhanga, kuwashambulia raia, na harakati za utekaji nyara kwa ajili ya fidia. Shambulio la bomu lililofanywa na AQIM mnamo mwaka 2007 dhidi ya jengo la makao makuu ya Umoja wa Mataifa na jengo la serikali ya Aljeria jijini Algiers liliwaua watu 60. Mnamo mwezi Januari mwaka 2016, AQIM ilishambulia hoteli moja nchini Bukinafaso ambalo liliwaua watu 28 na kuwajeruhi 56. Mnamo mwezi Machi, mwaka 2016, AQIM ilidai kuhusika na shambulio dhidi ya eneo maalum la mapumziko ya kitalii ufukweni Kodivaa ambalo liliwaua watu 16 na kuwajeruhi wengine 33. Mnamo Januari mwaka 2017, AQIM ilitekeleza shambulio la kujitoa mhanga ambalo liliwaua watu zaidi ya 50 mjini Gao, Mali.
Mnamo tarehe 27, mwezi Machi, mwaka 2002, Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Marekani ilitaja AQIM kuwa Kundi la Kigaidi la Kigeni chini ya kifungu 219 cha Sheria ya Uhamiaji na Uraia, kama ilivyorekebishwa. Hapo awali, mnamo tarehe 23, mwezi Septemba, mwaka 2001, AQIM iliorodheshwa kwenye Kiambatanisho cha cha Amri ya Rais 13224, na kutokana na hiyo, inakabiliwa na vikwazo chini ya Amri hiyo kama Gaidi wa Kimataifa Mwenye Sifa Maalumu. Matokeo yake ni kwamba, mali yote na maslahi ya AQIM katika mali, vyote vilivyoko chini ya mamlaka ya Marekani vimezuiwa, na watu wa Marekani kwa jumla wamekatazwa kushiriki kwenye miamala yoyote na AQIM. Ni kosa la jinai kutoa kwa makusudi, au kujaribu au kula njama ya kutoa, msaada wa nyenzo au rasilimali kwa AQIM.