Tuzo kwa Mahakama inaahidi kutoa tuzo ya hadi dola milioni saba kwa taarifa kumhusu Abu Ubaydah Yusuf al-Anabi, anayejulikana pia kama Abou Obeida Youssef al-Annabi na Yazid Mubarak. Al-Anabi ni kiongozi wa shirika la kigaidi la al-Qa’ida Kwenye Maghreb ya Kiislamu (AQIM). AQIM lilimtangaza al-Anabi kama kiongozi wake mpya mnamo mwezi Novemba, mwaka 2020. Al-Anabi aliahidi utii kwa kiongozi wa al-Qa’ida (AQ) Ayman al-Zawahiri kwa niaba ya AQIM’s na anatarajiwa kushiriki katika usimamizi wa kimataifa wa AQ.
Al-Anabi, ambaye ni raia wa Aljeria, awali alikuwa kiongozi wa Baraza la Watu Mashuhuri la AQIM na alitumika katika Baraza la Shura la AQIM. Al-Anabi alikuwa hapo zamani mkuu wa vyombo vya habari wa AQIM.
Mnamo tarehe 9 mwezi Septemba, mwaka 2015, Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Marekani ilimtaja al-Anabi kuwa Gaidi wa Kimataifa Mwenye Sifa Maalumu kuambatana na Amri ya Rais 13224, kama ilivyorekebishwa. Matokeo ya kutajwa huku, miongoni mwa matokeo mengine, ni kwamba mali yote na maslahi ya al-Anabi katika mali, vyote vilivyoko chini ya mamlaka ya Marekani vimezuiwa, na watu wa Marekani kwa jumla wamekatazwa kushiriki kwenye miamala yoyote na al-Anabi. Aidha, ni kosa la jinai kutoa kwa makusudi, au kujaribu au kula njama ya kutoa, msaada wa nyenzo au rasilimali kwa AQIM, kundi lililotajwa na Marekani kama Shirika la Kigaidi la Kigeni. Al-Anabi aliwekwa kwenye orodha ya vikwazo ya Azimio 1267 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSCR 1267) mnamo tarehe 29 mwezi Februari, mwaka 2016, hivyo kumfanya kukabiliwa na uwezekano wa mali yake kudhibitiwa kimataifa, kupigwa marufuku ya kusafiri, na vikwazo vya silaha.