Tuzo kwa Mahakama inaahidi kutoa tuzo ya hadi dola milioni tano kwa taarifa kumhusu Abu Huzeifa, anayejulikana pia kama Higgo, kwa kushiriki kwake kwenye shambulio la mwaka 2017 la Tongo Tongo, nchini Nijeri. Abu Huzeifa ni kamanda wa kundi la ISIS-Kanda Kubwa ya Sahara (ISIS-GS).
Mnamo tarehe 4 mwezi Oktoba, mwaka 2017, karibu na kijiji cha Tongo Tongo, nchini Nijeri, wapiganaji wenye uhusiano na ISIS-GS walishambulia wanachama wa kikosi cha Majeshi Maalumu ya Marekani kilichopewa jukumu la kufunza, kushauri na kusaidia majeshi ya Nijeri katika vita dhidi ya ugaidi. Shambulio hilo lilisababisha vifo vya wanajeshi wanne wa Marekani na wanne wa Nijeri. Wamarekani wawili zaidi na Wanijeri wanane walijeruhiwa katika pambano hilo. Mnamo tarehe 12 mwezi Januari, mwaka 2018, kiongozi wa ISIS-GS Adnan Abu Walid al-Sahrawi alidai kuhusika na shambulio hilo.